MRADI WA KUSWAHILISHA PROGRAMU HURIA

 

WARSHA YA ARUSHA 1-5 NOVEMBA 2004-11-22

 

 

 

MADA YA MAFUNZO

 

 

 

 

 

KATEGORIA ZA KISARUFI KATIKA UUNDAJI WA MANENO.

(GRAMMATICAL CATEGORIES IN TERM CREATION)

 

 

 

G. Mrikaria 

 

 

 

 

 

 

1.0 UTANGULIZI

 

Katika lugha yoyote kuna aina mbalimbali za maneno. Maneno haya yamepewa kategoria kulingana na matumizi yao au uhusiano baina ya aina moja ya maneno na aina nyingine za maneno.

 

Shughuli ya uundaji wa msamiati mpya imekuwa ikifanyika wakati wote binadamu alipokuwa akitumia lugha kufikisha ujumbe wake. Wakati wote amekuwa akitunga maneno mapya kueleza mambo au dhana mpya alizobuni au kuziona. Maneno haya yamekuwa yakiwakilisha vitu au vitendo alivyofanya au kusikia. Maneno yamekuwa yakiundwa mara yalipohitajika kwa kuwa hayakuwepo katika lugha. Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, dhana mbalimbali zimekuwa zikibuniwa na vitu vingi vimekuwa vikiundwa ambavyo havikuwepo katika utamaduni wa lugha husika, hivyo imelazimu vitafutiwe na kupewa maneno au majina ya kuviwakilisha.

 

Katika Kiswahili uundaji wa maneno hufanyika kwa njia mbalimbali. Njia ya kwanza ni ile ya kukopa maneno kutoka katika  lugha nyingine. Njia hii mara nyingi hufanyika kwa kutohoa maneno ya lugha nyingine na kuyapatia mazingira ya utamkaji katika Kiswahili, kwa mfano, televisheni limekopwa toka katika Kiingereza “television”, kompyuta limekopwa toka katika neno “computer”. Mifano hiyo michache inaonyesha jinsi njia hii ya uundaji wa maneno ilivyotumika katika Kiswahili.

 

Njia nyingine ni ile kuunda maneno mapya kwa kutumia njia ya uambishaji au unyambulishaji wa maneno yaliyo katika Kiswahili. Mfano neno cheza ukiliwekea kiambishi ku- unapata neno kucheza na  ukiweka kiambishi m- mwanzoni na kubadili kiambishi cha mwisho –a na kiambishi –o utapata neno mchezo. Njia hii imekuwa ikitumika sana katika Kiswahili ikitumika kama njia ya kuzalisha maneno kwa kutumia maneno yanayotumika katika lugha yenyewe bila kwenda nje ya lugha.

 

Njia nyingine ni ile ya kufupisha maneno marefu na kuunga silabi za mwanzo ili kupata neno moja mfano, chakula cha jioni kuwa cha- + jio = chajio. Pia inawezekana kuunganisha maneno mawili au zaidi ili kupata neno moja mfano pakashume, mbwa-mwitu nk.

 

Vilevile maneno yanaweza kuundwa kwa kubadili kategoria za maneno. Kwa njia hii tutaona jinsi kategoria za maneno mbalimbali zinavyotumika kuzalisha maneno ya kategoria nyingine.

 

2.0 Kategoria za kisarufi katika uundaji wa maneno

 

Katika utaratibu wa kuunda maneno mapya, moja ya njia itumikayo kuzalisha maneno mapya ni ile ya kuchukua neno lililo katika kategoria moja na kuunda neno au maneno ya kategoria kama hiyo au maneno ya kategoria nyingine. Njia hii imekuwa ikitumika sana katika uundaji wa maneno ya Kiswahili. Maneno yanaweza kuundwa kwa kuangalia sifa maalumu za vitu au matukio fulani yaliyotokea. Kutokana na kitendo kinachofanywa na kitu nacho kitu hicho huweza kupewa jina kulingana na kitendo hicho. Mfano kitendo anachofanya mdudu anayetoboa punje za mahindi au maharage, watu wameamua kusema kuwa anabungua, hivyo naye mdudu huyo  akapewa jina la bungua.

Neno baki ni kitenzi cha kinachoeleza hali ya mtu au kitu kutoondoka na pia ni nomino yenye maana ya salio.

chapa kama kitenzi humaanisha piga, na likitumiwa kama nomino humaanisha alama maalumu inayowekwa kwenye kitu au bidhaa.

Baadhi ya maneno yameonekana kuwa na uwezo wa kuzalisha maneno mengine na yale maneno yaliyozalishwa nayo yameweza kuzalisha maneno ya aina nyingine. Kwa hali hiyo tumeyaita yale maneno yaliyozalishwa moja kwa moja kutoka maneno ya msingi kuwa yamezalishwa katika hatua ya kwanza. Yale maneno yaliyozalishwa kutokana na maneno yaliyozalishwa katika hatua ya kwanza tumeyaita maneno yaliyozalishwa katika hatua ya pili. Iwapo yatapatikana maneno yatakayozalishwa kutokana na maneno yaliyozalishwa katika hatua ya pili tutayaita maneno yaliyozalishwa katika hatua ya tatu.

Sasa hebu tuangalie jinsi ambavyo aina mbalimbali za maneno zinavyoweza kutumika kuzalisha maneno mengine.

 

2.1 Uundaji wa maneno kwa kutumia vitenzi

 

Vitenzi ni aina ya maneno yenye uwezo mkubwa kuliko maneno mengine kushiriki katika utaratibu wa kuunda maneno mengine. Kitenzi kimoja kinaweza kutumika kuunda maneno ya kategoria mbalimbali kama vile nomino, vielezi, vivumishi nk.

 

1. Kitenzi sikia kinaweza kuzalisha maneno kadhaa katika hatua mbalimbali. Kinaweza kuzalisha maneno katika hatua ya kwanza, ya pili na kuendelea kama ifuatavyo:

hatua ya kwanza kinaweza kuzalisha maneno kama vile: msikiaji, sikio, usikivu, sikiliza.

msikiaji (nm) - mtu anayesikia

sikio (nm) – kiungo cha mwili kinachofanya kazi ya kusikia

usikivu (kl) – hali au tabia ya kusikia

sikiliza (kt) – pokea na dhibiti mawimbi ya sauti kwa umakinifu.

 

Katika hatua ya pili maneno yaliyozalishwa kutokana na neno la msingi nayo yanaweza kuzalisha maneno mengine, kwa mfano maneno yafuatayo yanaweza kuzalisha maneno kama ifuatavyo:

sikiliza linaweza kuzaa maneno kama vile: msikilizaji na usikilizaji, masikilizano.

msikilizaji (nm) – mtu anayesikiliza

usikilizaji (nm) – kitendo cha kusikiliza

masikilizano (nm) – maelewano.

 

2. kitenzi tembea kwa hatua ya kwanza kinaweza kuzalisha maneno kama vile: mtembeaji, tembelea, tembeza, n.k.

mtembezi – mtu mwenye tabia ya kutembea ovyo

utembeaji – jinsi au namna ya kutembea

utembezi – tabia ya kutembea ovyo

matembezi – kitendo cha kutembea rasmi.

tembelea – enda mahali kwa makusudi ya kumwona mtu au jambo fulani

Katika hatua ya pili maneno yafuatayo yanaweza kuzalisha maneno mengine kama ifuatavyo:

tembelea – tembeleana, tembeleka, tembeleo, utembeleaji, matembeleano

tembeza - mtembezi, utembezi, matembezi, utembezaji, mtembezaji, tembezwa, tembezana.

 

3. kitenzi cheza kwa hatua ya kwanza kinaweza kuunda maneno yafuatayo: mchezo, uchezaji, mchezaji, mcheza, chezesha, chezwa.

mchezo – jambo au tendo lifanywalo kwa ajili kuleta furaha au hufanywa na zaidi ya mtu mmoja kwa ajili ya mashindano

uchezaji - kitendo cha kucheza

chezesha ­– simamia mchezo

mcheza – mtu anayecheza

mchezaji – mtu anayecheza mchezo

katika hatua ya pili maneno yafuatayo yanaweza kuzalishwa kutokana na neno lililozalishwa katika hatua ya kwanza kama ifuatavyo:

chezesha – mchezeshaji, uchezeshaji

 

4 tafuta kwa hatua ya mwanzo linaweza kuzalisha maneno kama vile: utafutaji, mtafutaji

utafutaji – kitendo cha kutafuta

mtafutaji – mtu anayetafuta

 

5 kokota ­– mkokota, mkokoto, mkokotoo, mkokotoaji, mkokotaji

 

6 cheka kwa hatua ya kwanza linaweza kuzalisha maneno kama vile chekesha, kicheko, cheko, chekea, chekwa, ucheshi, mcheshi, n.k.

Katika ya pili neno lililozalishwa katika hatua ya kwanza linaweza kuzalisha maneno mengine mfano, chekesha – mchekeshaji, uchekeshaji, kichekesho, chekeshea, chekeshwa

 

Utaona kuwa vitenzi vinavyozalishwa kutokana na vitenzi vingine vinakuwa na uwezo zaidi wa kuzalisha maneno mengine kuliko kategoria nyingine ya maneno.

 

 2.2 Kutumia Nomino kuunda maneno mengine

 

Nomino pia huweza kuzalisha maneno ya kategoria sawa nazo na pia maneno ya kategoria nyingine, kwa mfano:

 

taifa – taifisha, utaifishaji, taifishwa, taifisho

buku – bukua

taabu – taabisha, utaabishaji, taabika

sakafu – sakafu, sakafia, sakafisha, usakafishaji, msakafishaji

 

2.3 Uundaji wa maneno kwa kutumia vivumishi

 

Vivumishi ni kategoria nyingine ya maneno inayoweza kuzalisha maneno ya aina nyingine, mfano:

refu – refusha, urefu, marefu, refuka, kwa hatua ya kwanza na kwa hatua ya pili: refusha inaweza kuzalisha maneno: urefushaji, marefusho, refushia, mrefushaji

nene – nenepa

Kwa hatua ya pili nenepa inaweza kuzalisha – unenepaji, nenepesha

Kwa hatua ya tatu nenepesha inaweza kuzalisha – unenepeshaji, unenepeshwaji, mnenepeshaji

safi – safisha, usafi, safisho kwa hatua ya kwanza

Kwa hatua ya pili usafi inaweza kuzalisha – usafishaji, msafishaji

zuri – mzuri, uzuri

pole – mpole, upole

bora – ubora, boresha, uboreshaji, maboresho, boreka

 

2.4 Uundaji wa maneno kwa kutumia vielezi

 

Vielezi ni kategoria ya maneno ambayo huweza kuunda maneno ya aina nyingine. Kutokana na kielezi tunaweza kuunda maneno mbalimbali na ya kategoria tofauti, Mfano:

haraka – harakisha. Hapa kitenzi harakisha kimeundwa kutokana na kielezi haraka.

Kwa hatua ya pili harakisha inaweza kuzalisha neno uharakishaji, harakisho  

tayari – tayarisha, utayari kwa hatua ya kwanza  ya uzalishaji

Kwa hatua ya pili ya uzalishaji tayarisha inazaa – utayarishaji, mtayarishaji, matayarisho

karibu - kwa hatua ya kwanza inazalisha – ukaribu, karibia, karibisha na kwa hatua ya pili neno karibisha linaweza kuzalisha – makaribisho, ukaribishaji, makaribishano, karibishana, karibishia

binafsi linaweza kuzalisha – ubinafsi, binafsisha, ubinafsishaji

 

2.4 Kuunganisha maneno mawili au zaidi kuunda neno moja

 

Mara nyingine hutokea dhana au kitu kipya ikashindikana kupatiwa neno moja fupi litakalofikisha ujumbe au kuwakilisha dhana husika. Kwa kawaida njia inatumiwa katika kuunda maneno yenye kuleta utata kama huu kwa kuunganisha maneno mawili au zaidi yenye kuhusika ili kuleta maana. Uunganishaji wa maneno kama haya unaweza kufanyika kwa kuunganisha nomino na nomino, nomino na kivumishi au kitenzi na nomino, n.k.

 

2.4.1 Nomino + nomino

 

Nomino mbili zinaweza kuunganishwa ili kuunda neno moja lenye kuwakilisha dhana moja ambayo katika lugha imeshindikana kupata neno moja litakaloweza kuiwakilisha, mfano:

 

mwana + mke – mwanamke

mwana + maji – mwanamaji

mwana + kondoo – mwanakondoo

mwana + sheria - mwanasheria

mbwa + mwitu – mbwamwitu

paka + shume - pakashume

kiazi + ulaya – kiaziulaya

kiazi + kitamu – kiazikitamu

kidole + tumbo - kidoletumbo

mwana + mwali - mwanamwali

mwana + nchi – mwananchi – mwenyeji wa nchi fulani

viwavi + jeshi – viwavijeshi

hifadhi + data – hifadhidata

eneo + data – eneodata

kanzi + data - kanzidata

 

2.4.2 nomino + kivumishi

 

Nomino huweza kuunganishwa na kivumishi ili kuunda neno moja. Mifano ifuatayo inaweza kudhihirisha usemi huu.

mwana + kwetu – mwanakwetu - jamaa

mwana + mkiwa – mwanamkiwa - yatima

mwana + haramu – mwanaharamu – mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa

jua + kali - juakali

 

2.4.3 nomino + kielezi

 

mcheza + kwao – mchezakwao

Miji + kenda – Mijikenda

mkwaju + nyuma – mkwajunyuma

mkwaju + mbele - mkwajumbele

 

2.4.4 kitenzi + nomino

Kitenzi kinaweza kuunganishwa pamoja na nomino ili kuunda neno jipya. Katika Kiswahili kuna maneno kadha yaliyoundwa kwa njia hii, mfano:

chemsha + bongo – chemshabongo -

mpiga + mbizi – mpigambizi – mzamaji chini ya maji

komba + mwiko – kombamwiko – aina ya ndege; mende

komba + moyo – kombamoyo – mti unaotumika kuezekea paa la nyumba

chekea + mwezi – chekeamwezi – aina ya ndege; kipila

 

2.4.5 Urudufishaji wa maneno

 

Njia ya urudufishaji wa maneno hutumika pia sana kwa kurudia neno moja mara mbili. Mifano ni maneno kama vile:

piga linaweza kuzalisha neno - pigapiga

kata linaweza kuzalisha neno - katakata

choma - chomachoma

ponda - pondaponda

legea - legalega - kosa kuwa imara

 

 

2.4.6 Kufupisha kikundi cha maneno ili kupata neno moja

 

Njia mojawapo inayotumika katika uundaji wa maneno ni kufupisha kikundi cha maneno ili kupata neno moja. Njia hii hutumika zaidi katika kuonyesha kifupi cha majina ya mashirika, magonjwa au hata dhana fulani, mfano:

Upungufu wa Kinga Mwilini – UKIMWI

Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili – TUKI

Chama cha Mapinduzi – CCM

Chakula cha jioni – chajio

Taasisi ya Kiswahili na Lugha za Kigeni – TAKILUKI

Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI 

Chama cha Netiboli Tanzania – CHANETA

Kampuni ya Mabasi ya Taifa – KAMATA

Sarufi Maumbo ya Kiswahili Sanifu – SAMAKISA

Sarufi Miundo ya Kiswahili Sanifu – SAMIKISA

Fonolojia ya Kiswahili Sanifu – FOKISA

 

Hivyo kwa kutumia njia utaona kuwa dhana inayowakilishwa na mlolongo mrefu wa maneno inakuwa rahisi kutajwa kwa kutumia neno moja lililofupishwa.

 


MAREJEO

 

  1. Massamba D.P.B. na wenzake (1989) Uundaji wa Istilahi katika Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili (Makala za Semina ya Kimataifa ya Usanifishaji wa Istilahi za Kiswahili: Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili.
  2. Massamba D.P.B., Kihore Y.M., Msanjila Y.P. (2001); Sarufi Maumbo ya Kiswahili: TUKI.
  3. Mathews, P.H. (1974); Morphology: An Introduction to the Theory of Word Structure, Cambridge University Press, Cambridge.
  4. Mdee J.S. (1986) Kiswahili; Muundo na Matumizi yake: Intercontinental Publishers Ltd.
  5. Mdee J.S. (1999) Sarufi ya Kiswahili; Sekondari na Vyuo: Dar es Salaam University Press (1996) Ltd.
  6. Simeon Potter (1950) Our Language: Hanzel Watson & Viney Ltd