MRADI WA KUSWAHILISHA PROGRAMU HURIA

 

WARSHA YA ARUSHA 1-5 NOVEMBA 2004-11-22

 

 

 

MADA YA MAFUNZO

 

 

 

UUNDAJI WA ISTILAHI: UZOEVU WA BARAZA LA KISWAHILI LA TAIFA (BAKITA)

 

na

 

 P.C.K. Mtesigwa

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

UUNDAJI WA ISTILAHI: UZOEVU WA BARAZA LA KISWAHILI LA TAIFA (BAKITA)

 

1.0 Utangulizi

 

Jukumu kuu ambalo Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA) limepewa kisheria kwa mujibu wa Sheria ya Bunge Na. 27 ya mwaka 1967 iliyoliunda ni kukuza, kuimarisha na kuendeleza Kiswahili hasa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Katika marekebisho ya sheria hiyo yaliyofanyika mwaka 1983 kwa Sheria ya Bunge Na. 7, BAKITA limepewa uwezo wa kufuatilia na kusaidia ukuzaji wa Kiswahili katika nchi za nje pia. Kwa hiyo kazi zinapokuwa zimethibitishwa na BAKITA huzihusu pia juhudi za uendelezaji wa Kiswahili katika nchi za nje.

Kimsingi ukuzaji au uimarishaji wa lugha maana yake, kwa upande mmoja, ni utumiaji wa lugha hiyo kwa usahihi.  Kwa mtazamo huo maana yake ni kuhakikisha kwamba  kanuni za sarufi yake zinafuatwa. Lakini pamoja na hilo, kwa upande mwingine kuna suala la kuiwezesha lugha hiyo kukidhi mahitaji ya watumiaji wake wa kila hali na kila uwanja wa matumizi. Kusema kweli mojawapo ya vigezo vinavyotumika kujua kiwango cha kukomaa kwa lugha ni kupima jinsi inavyojimudu katika msamiati wake kukidhi matumizi katika nyanja mbalimbali zikiwemo nyanja maalumu za kitaalamu. Ili kutimiza lengo hilo hapan budi msamiati wake ukuzwe na kusambaa. Kwa mujibu wa Mkude (2004) aina ya msamiati uliosukwa kimkakati na kuratibiwa kwa nia ya kuashiria dhana teule za taaluma fulani huitwa istilahi. Huu ni msamiati maalumu ambao umetokana na msamiati mpana wa lugha na kufanyiwa marekebisho ili kuhakikisha kwamba maana ya neno inaacha au inapanua maana yake ya kawaida na kubeba maana maalumu kwa ajili ya matumizi katika uwanja maalumu.

Ili kutekeleza majukumu yake kama chombo chenye mamlaka ya kukuza na kuimarisha Kiswahili kama lugha ya taifa na mojawapo ya lugha mbili rasmi za Tanzania, BAKITA linayo idara mahususi (Idara ya Kamusi na Istilahi) inayoshughulikia kusanifu istilahi kwa ajili ya kuziba pengo la kukosekana kwa istilahi katika nyanja mbalimbali. Kazi kubwa inayofanywa na idara hii ni kutafuta visawe vya Kiswahili vya istilahi za Kiingereza zilizopo tayari. Katika kufanya kazi hiyo BAKITA hupokea orodha za istilahi kama hizo baadhi huja tayari na mapendekezo ya visawe vya Kisahili vilivyopendekezwa na mletaji mwenyewe ili yapitiwe na kurekebishwa kama hapana budi au yathibitishwe ili baada ya kukubaliwa rasmi na BAKITA yasambaazwe na kuanza kutmika. Lakini kwa kiasi kikubwa orodha zinazoletwa huwa hazina mapendekezo yoyote ya visawe vya Kiswahili. Idara husika hufanya utafiti kutafuta visawe na kasha Kamati ya kuisanifu istilahi ya BAKITA hukaa na kutumia mbinu mbalimbali ili kuvipitia na kuvisanifu visawe hivyo. Ndipo visawe hivyo vinapowaslishwa katika kikao cha Baraza zima ili kutoa idhini na hatimaye kuvisambaza vianze kutumika. Mpaka sasa BAKITA limefaulu kusanifu na kusambaza istilahi zipatazo zaidi ya elfu 10 za nyanja maalumu na taaluma mbalimbali zaidi ya 30. 

Lengo la makala hii ni kueleza misingi na mbinu ambazo BAKITA hutumia katika kuunda istilahi za Kiswahili. Vilevile makala itagusia matatizo yanayojitokeza wakati wa kuunda istilahi na pia baada ya kuunda istilahi.

 

2.0 Misingi na mbinu za uundaji wa istilahi

Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO) ambalo miongoni mwa kazi zake ni kuratibu na kusimamia uendelezaji wa istilahi kimataifa, limeorodhesha kanuni zinazopaswa kufuatwa wakati wa kuunda istilahi katika lugha yoyote. Misingi hii imetokana hasa na mtazamo wa wanaisimu wa Vienna – yaani “Shule ya Istilahi ya Vienna (Austria)” iliyoanzishwa na Eugen Wuster. Kwa muhtasari kanuni hizo zinahusu uundaji wa istilahi lugha moja tu inapohusika na pale lugha mbili zinapohusika. Lugha moja inapohusika kanuni zifuatazo hazina budi  zizingatiwe:

(1)   Istilahi ziundwe baada ya kupata dhana iliyoelezwa kwa ukamilifu na wazi.

(2)   Istilahi ziwe fupi kadiri iwezekanavyo lakini zenye kueleweka. Uundaji wa istilahi kwa vifupisho na akronimia uepukwe hasa kama istilahi kamili si ndefu sana.

(3)   Sarufi ya lugha inayohusika lazima itiliwe maanani. Kwa hiyo istilahi ziundwe kwa kufuata mofolojia ya kawaida ya lugha.

(4)   Istilahi ziundwe kwa njia ambayo itakuwa rahisi kuunda istilahi nyingine kwa mnyumbuliko.

(5)   Uundaji wa istilahi kwa kupanua maana ya neno uepukwe hasa iwapo nyanja zinazotumia maneno hayo zinakaribiana, ili kuepusha utata. Kwa hiyo mfumko wa sinonimia au homonimia (visawe) hauna budi kuepukwa ili watumiaji wasikanganyikiwe.

Lugha mbili zinapohusika kanuni zifuatazo zizingatiwe:

(1) Uundaji wa istilahi kwa njia ya kukopa (kutohoa) maneno ya lugha nyingine uzingatie kuchukua maneno kama yalivyo katika lugha ya asili na kufanya marekebisho machache tu ili kulingana na sarufi na matamshi ya lugha pokezi.

(2) Uundaji wa istilahi kwa kutumia Kigiriki na Kilatini uendelezwe ili kuzingatia uwakilishi sahihi wa dhana hasa za sayansi na pia kupunguza kishawishi cha kupendelea kutumia baaadhi tu yalugha zinazotumika ulimwenguni hivi sasa.

Katika uzoevu wa kusanifu istilahi, BAKITA limekuwa likizingatia pia kanuni za nyongeza ili kupata ufanisi zaidi kwa kutilia maanani jamii ya watumiaji wa Kiswahili na utamaduni wake. Kubwa kati ya kanuni hizo za nyongeza ni:

(1)   istilahi ziepuke utusani – yaani zisiundwe kwa maneno ambayo tayari yanaeleweka kwamba ni matusi kwa watumiaji. Kwa mfano katika kutafuta kisawe cha penis, neno mboo hushitua watumiaji wa Kiswahili wengi na badala yake neno dhakari huvumulika na kutumika zaidi. Kadhalika  kisawe cha neno bone marrow neno uboho ingawa ni sanifu pia lakini huepukwa sana katika matumizi na badala yake neno uloto limekomaa sana katika matumizi. Vilevile katika kutafuta kisawe cha neno anus, neno mkundu hushitua watumiaji na neno ngoko likachukuliwa.

(2)   Istilahi ziwe angavu vya kutosha – yaani istilahi ziweze kudokeza dhana liliyokusudiwa kwa kina na usahihi kadiri iwezekanavyo. Wakati wa kutafuta kisawe cha neno flip chart kwa Kiswahili kumekuwa na pendekezo la neno bango kitita. Katika kulichambua neno hilo imedhihirika ya kwamba ingawa neno bango kwa kiasi fulani linawakilisha ukubwa wa chart lakini dhana ya flip haijidhihirishi. Hivyo halina uangavu wa kutosha. Pendekezo linaloelekea kupendelewa ni chati pindu kwa kuwa neno hilo linawakilisha dhana ya chart na pia utumiksji wake wa kupinduliwa wakati chati hiyo inapotumiwa.

(3)     Istilahi ziwe na ulinganifu wa mtiririko ulio katika dhana za kikoa kimoja. Katika hili ni muhimu kwa wasanifishaji kukumbuka kwamba istilahi hazikai pekepeke. Hazifiki mbali iwapo zitasimama pasipo kuhusisha maneno mengine yaliyo katika uga huo. Istilahi ni kama matundu ya wavu ambayo kila moja sharti ligusane na lenzake ili hatimaye mfumo mzima wa wavu uweze kutengenezwa. Kwa hiyo istilahi moja iwe chanzo cha kupata istilahi zingine kutokana na kuinyumbulisha na kuunda istilahi zinazohusiana katika uwanja ule. Kwa mfano: Sumaku (magnet), Usumaku (magnetism), Sumakisha (magnetise), Jisumakisha (auto magnetise), Usumakishaji (magnetization, nk.

(4)   Istilahi zilizozoeleka au kukomaa kutokana na kutumika kwa muda mrefu zisibadilishwe. Kanuni hii ni muhimu sana katika ukubalifu wa istilahi zinazoundwa. Ni muhimu kabla ya kuunda istilahi mpya kuchunguza iwapo hakuna istilahi inayotumika tayari ambayo inawakilisha kw usahihi dhana inayokusudiwa. Uzoevu wa BAKITA umeonyesha kuwa ni vigumu kwa istilahi mpya kukubaliwa na kushamiri pale ambapo tayari kulikuwa na istiahi zilizokuwa zikitumika, hasa zile za muda mrefu. Kwa mfano neno Ovataimu (overtime) lililokuwa limezoeleka kwa muda mrefu limeendelea kutumika badala ya neno ajari. Vivyo hivyo neno Mdai (creditor) limeendelea kutumika badala ya neno Mwia. Maneno yote mawili ni ya siku nyingi lakini neno mdai limezagaa zaidi katika matumizi kuliko neno mwia.

 

3.0 Vyanzo vya istilahi

BAKITA linafuata utaratibu ufuatao ili kupata istilahi sanifu:

(a) Hazina ya Kiswahili chenyewe

Hazina ya Kiswahili chenyewe huhusisha Kiswahili na lahaja nyingine za Kiswahili. Kwa kawaida kabla ya kutafuta kisawe cha Kiswahili cha istilahi iliyo katika lugha ngeni, wataalamu wa uwanja husika huhusishwa kikamilifu ili kueleza kwa ukamilifu dhana au maana ya istilahi hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya Kusanifu Istilahi. Baada ya hapo wajumbe huanza kutafuta iwapo kuna kisawe katika Kiswahili Sanifu cha istilahi iliyotolewa. Kama kisawe hakipatikani katika Kiswahili Sanifu wajumbe hutafuta kama kuna neno katika lahaja za Kiswahili. Mifano michache jinsi mbinu hii ilivyotumika ni istilahi zifuatazo:

Chovyo (oedema) kutoka lahaja ya Kipemba

Mbolezi (elegiac poetry) kutoka lahaja ya Kimvita

Ng’ozi (leaf curl) kutoka lahaja ya Kimtang’ata 

Kisabeho (breakfast) kutoka lahaja ya Kipemba (kutokana na Kitenzi kusabehe)

Kiangata (hob) kutoka lahaja za Kiamu na Kisiu

Hazina ya Kiswahili chenyewe pia huhusu mbinu mbalimbali zinazoweza kuunda maneno ya Kiswahili kwa njia ya kunyumbulisha mzizi waneno, kufinyaza maneno au kwa njia ya kuunganisha maneno:

Finyazo

Chakula cha jioni = Chajio

Chemchemi ya maji moto = Chemimoto

Mfupa wa paja = Fupaja

Hati ya kukataza kuiga = Hataza

Bara lililozama = Barazama

Matuta kama ngazi = Matungazi

Huduma hadi bandarini = Huhaba

Huduma hadi melini = Huhame

Utando mwembamba wa ogani = Utandogani

Teknolojia ya habari na mawasiliano = Teknohama nk.

Jambo la kuzingatia ni kwamba mbinu hii inapaswa itumiwe kwa uangalifu sana ili istilahi itakayotokana nayo iwasilishe dhana kwa usahihi na pia iwe na uangavu wa kutosha kwa watumiaji. Kama mojawapo kati ya sifa hizo ikipuuzwa istilahi haitakuwa sahihi ipasavyo na wala uangavu ukipuuzwa istilahi haitapata nguvu ya kusambaa na kushika mizizi baina ya watumiaji.

Muunganiko wa maneno

Mbinu hii hutumika hasa kwa lengo la kufupisha istilahi ndefu kwa kuondoa viunganifu au umilikaji.

Kipima pembe kwa ubapa = Kipimapembe ubapa

Doa la kutu = Doakutu

Nyundo ya rungu = Nyundorungu

Mwana + harakati = Mwanaharakati

Mwendo wa kasi = Mwendokasi

Nishati iliyotulia = Nishati tuli

Nishati yenye mwendo = Nishati mwendo

 (b) Hazina ya lugha za Kiafrika

Lugha za Kiafrika ni chanzo kingine ambacho husaidia kuunda visawe vya Kiswahili. Hazina hii hutumiwa pale hazina ya Kiswahili chenyewe inaposhindwa kukidhi haja ya kupata istilahi mwafaka inayoweza kuwakilisha dhana inayoshughulikiwa. Upendeleo hutolewa kwanza kwa lugha za Kibantu kwa sababu Kiswahili chenyewe ni mojawapo kati ya lugha za kundi hilo. Kwa hiyo maneno yanayotoka katika lugha za kundi hili hata yachukuliwapo katika Kiswahili yatakuwa na uangavu wa kutosha kwa watumiaji wa Kiswahili. Kwa sasa BAKITA limekuwa likitafuta maneno yaliyo katika lugha za Kibantu za Tanzania kuliko za nchi zingine. Jambo la kuzingatia kamam ilivyokwisha kudokezwa katika kanuni ya kukopa au kutohoa ni kwamba maneno yanayochukuliwa kutoka huko hurekebishwa ili yatii kanuni ya muundo wa Kiswahili hasa katika maumbo yake na pia jinsi yanavyopaswa yapatanishwe yatumikapo katika sentensi. Mifano michache kutoka hazina hii ni kama ifuatayo:

Neno la asili                           Istilahi Kisw)         Umoja (Kisw)  Wingi   Upatanisho

Lishiganga (Kisukuma)         Shiganga (boulder)      Ř                    Ma-     li-     ya-

Akasoko (Kinyakyusa)          Kasoko (cardella)        N-                    N-      I-      zi-

Olweya (Kihaya)                    Lweya (plain land)       N-                   N-      I-      zi

Itepo (Kimwera)                    Tepo(clone)                    Ř                   Ma-    A-    wa-

                                                                 au pia                                  N-      I-      zi-

Ulugiligili (Kinyakyusa)       Giligili (synovial fluid)    N-                 N-      I-      zi-

Lugha zingine za Tanzania ambazo si za Kibantu pia zimetoa mchango wa kupata istilahi za Kiswahili. Utaratibu unaofuatwa umekuwa ni uleule wa kuchukua neno la asili na kulirekebisha ili lichukue umbo na kanuni za sarufi ya Kiswahili. Mifano michache iliyotokana na hazina hiyo ni kama ifuatayo:

Embuti (Kimasai)        Mbuti (Kiswahili) duodenum

Engalem (Kimasai)      Ngalemu (Kiswahili) carving knife

Kamongo (Kijaluo)      Kamongo (Kiswahili) cat fish nk

Hazina ya lugha za Kiafrika pia imehusisha lugha zisizo za Kibantu zinzazotumiwa nje ya Tanzania. Mpaka sasa mchango uliopatikana umetoka katika baadhi ya lugha za Afrika Magharibi. Mifano michache iliyotokana na lugha hizo ni kama ifuatayo:

 Kola (Kihausa, Kiibo, Kiyoruba)            Kola (Kiswahili) kola nut

Rara (Kiyoruba)                                        Rara(Kiswahili) ballad

Dyeli (Kimaninke, Kisusu)                       Yeli (Kiswahili) griot

Juju (Kiyoruba, Kiibo, Kipijini)                Juju (Kiswahili) complex witchcraft nk

(c) Lugha za Kigeni

Sehemu kubwa sana ya istilahi za Kiswahili imetokana na Kiingereza na Kiarabu. Lugha zote hizi mbili zimekiathiri sana Kiswahili katika uwanja huu na msamiati kwa jumla kutokana na sababu za kihistoria kwamba pamekuwa na uhusiano wa kutawala na kutawaliwa. Maneno mengi mno ya Kiingereza na Kiarabu yametoholewa katika Kiswahili, hata pasipokuwa na sababu za kutosha, kiasi kwamba baadhi ya wataalamu hushuku kwamba lazima Kiswahili kiachane na tabia hiyo kwa kujitahidi kutazama hazina iliyo ndani ya Kiswahili chenyewe au katika lugha za Kiafrika.

Kama ilivyokiwsha kudokezwa kinachofanyika wakati wa kutumia hazina kutoka lugha hizi mbili ni kurekebisha maneno ya lugha hizo ili yakubaliane na mfumo wa matamshi na othografia ya Kiswahili. Mifano michache kati ya mingi tuliyo nayo ni kama ifuatayo:

Psychology = Saikolojia

Commissioner = Kamishena

Oxygen = Oksijeni

Hormone = Homoni

Element = Elementi

Vitamin = Vitamini

Uterus = Uterasi (Mji mimba)

Chocolate = Chokoleti/ chakleti

Chlorine = Klorini  nk.

Kwa kuchunguza orodha ya istilahi za Kiswahili iliyopo inaelekea utohoaji wa maneno ya Kiingereza na Kiarabu ndicho chanzo kikuu cha istilahi za Kiswahili badala ya kwamba hazina ya Kiswahili chenyewe inapaswa kuwa ya kwanza ikifuatwa na hazina ya lugha za Kiafrika.Ziko sababu nzuri tu wakati mwingine wa kuhitaji kuendeleza ukubalifu wa istilahi kimataifa. Yako maneno ambayo kwa mfano majina ya waasisi wa uvumbuzi Fulani ndiyo pia istilahi ya kitajwa kinachohusika. Lakini maneno hayo si mengi sana katika maarifa ya utaalamu wenyewe. Waswahili hawana budi kuchungua vyanzo vyao kikamilifu kwanza kabla ya kukkimblia kutohoa. Kanuni za unyambulishaji wa maneno, uhusianishaji wa dhana katika kikoa kimoja uwe ndilo jambo la kuzingatia awali ya yote katika usanifishaji wa istilahi.  

 

4.0 Matatizo

Ingawa misingi na mbinu zilizotajwa zimesaidia sana kupata na kusanifisha visawe  vingi vya Kiswahili lakini yapo matatizo yaliyojitokeza katika kutekeleza kazi hiyo. Hapa yataelezwa machache angalau kwa kifupi ili inapobidi hadhari ichukuliwe. Kimsingi matatizo haya yanagusia utumiaji wa hazina ya Kiswahili chenyewe na lahaja zake na hata lugha za Kiafrika, suala la kutumia finyazo kama mbinu ya kuunda istilahi na utusaji.

Hazina ya Kiswahili na lugha za Kiafrika

Kwa utaratibu ambao BAKITA limejiwekea ili kupata istilahi, Kiswahili chenyewe na lahaja zake ndiyo hazina ya kwanza. Lakini hazina hii haijatumika kikamilifu inavyopaswa kwa sababu mbalimbali. Lugha za Kiingereza na Kiarabu zimetagaa sana katika uundaji wa istilahi kwa sababu lugha hizi ziliwahi kuwa lugha za watawala nchini mwetu na zikapata hadhi ya pekee. Waundaji wa istilahi huziona kama kimbilio ili kurahisisha kazi yao kwa kutohoa istilahi zinazoletwa katika orodha. Laiti utafiti wa kutosha katika uwezekano wa kunyumbua maneno ya Kiswahili chenyewe, au kuchekecha msamiati ulio katika lahaja za Kiswahili ingeshangaza jinsi hazina ya Kiswahili ilivyo pana na ilivyo na uwezo wa kuziba mapengo yaliyopo ya istilahi. Kadhalika hazina kubwa bado inalala tuli katika lugha za Kiafrika hasa zikichambuliwa kwa kuzingatia mazingira ya kijiografia au shughuli za kiuchumi katika maeneo zinamozungumzwa.

Mbinu ya kutumia finyazo

Kama ilivyokwisha kudokezwa, uundaji wa istilahi kwa kutumia finyazo hauna budi ufanywe kwa makini sana ili istilahi iwakilishe kwa usahihi dhana inayokusudiwa na wakati huohuo iwe angavu ili watumiaji waweze kupata angalau fununu ya dhana hiyo. Baadhi ya mifano tuliyoitoa awali katika kueleza mbinu hii yaweza ktumika hapa ili kudhihirisha ugumu wa kuitumia.

Chemchemi ya maji moto = Chemimoto (Je, dhana ya maji imewakilishwa?)

Huduma hadi bandarini = Huhaba (Je, istilahi hii ni angavu vya kutosha kuwapa watumiaji fununu ya dhana inayowakilishwa?)

Utando mwembamba wa ogani = Utandogani (Je, dhana ya mwembamba imewakilishwa katika istilahi hii?)

Ushiriki katika hali ya mtu mwingine (empathy) = Ushirikali (Je, istilahi hii inazingatia hali ya mtu mwingine? Je, inao pia uangavu unaokusudiwa?)

Pengine jambo la msingi ni kuzingatia kwamba istilahi ni neno maalumu kwa dhana maalumu na hivyo suala la uangavu halipaswi kutiliwa mkazo sana. Lakini kama hivyo ndivyo, basi ni bora kuepuka finyazo na kutafuta mbinu nyingine itakayoweza kukidhi haja hiyo kwa ukamilifu zaidi.

Utusani

Sayansi inataka dhana iwakilishwe kikamilifu bila hoja ya mzungukozunguko. Koleo liitwe koleo na si kitu kingine. Hali hiyo inadai utamaduni wa watumiaji wa lugha, wakiwemo watumiaji wa Kiswahili, wasiyaonee aibu maneno ambayo yanaweza kuwa matusi katika matumizi ya kawaida. Zaidi ya hayo ili kutimiza lengo la kuunda istilahi maneno ambayo pengine ni matusi katika lugha ambayo si Kiswahili hayapaswi kutazamwa kama matusi katika lugha hiyo au katika Kiswahili chenyewe.

 

 

 

 

 

 

MAREJEO

BAKITA (1974 – 1983). Istilahi Sanifu (Namba 1 – 5)

 

BAKITA (1979). KAKULU (Kamati ya kusanifu Lugha) Na.3

 

ISO (1968). R 704-1968. Naming Principles

 

Kiingi, K. B. (1981). Swahilization of International Scientific Vocabulary (Mimeo)

 

Mkude, D. J. (2004). “Usuli na Umuhimu wa Istilahi katika Maendeleo ya Jamii” Makala iliyowasilishwa katika Warsha ya Mafunzo ya Uundaji wa Istilahi za Mradi wa Istilahi za Mikrosofti, Juni 2004, Dar es Salaam. Haijachapishwa

 

Mtesigwa, P.C.K. (1983). Ethnolects as a source of Swahili technical terms: A case of Kikerewe fisheries terminology. Tasnifu ya MA (Linguistics), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Haijachapishwa

 

Mwansoko, H. J. M. (2004). “Misingi ya Uundaji wa istilahi” Kitini kilichowasilishwa katika Warsha ya Mafunzo ya Uundaji wa Istilahi za Mradi wa Istilahi za Mikrosofti, Juni 2004, Dar es Salaam. Haijachapishwa