MRADI WA KUSWAHILISHA PROGRAMU HURIA

 

 

 

WARSHA YA ARUSHA 1-5 NOVEMBA 2004.

 

MADA YA MAFUNZO

 

 

MAANA KATIKA UUNDAJI WA ISTILAHI (MEANING IN TERMINOLOGY DEVELOPMENT)

 

 

S.S. SEWANGI

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 


 

 

 

Mada hii ya mafunzo umegawanyika katika sehemu zifuatazo:

 

UTANGULIZI

-         mkondo ya uundaji istilahi

-         mazingatio katika uundaji wa istilahi

 

AINA ZA MAANA

-         maana ya jumla

-         maana maalumu

-          

MAZINGATIO KATIKA UUNDAJI ISTILAHI

-         uwanja wa maarifa

-         waundaji istilahi

-         lengo la uundaji istilahi

-          

MAANA KATIKA LUGHA

-         maana ya jumla

-         maana maalum

 

MAANA KATIKA ISTILAHI

-         uhusiano wa kimaana

-         mbinu za ufafanuzi

-          

MAANA NA UUNDAJI WA VISAWE

-         mikabala ya kuunda visawe.

 

HITIMISHO

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

 

1.0 Mikondo ya uundaji wa Istilahi

 

Kazi ya uundaji istilahi mpya hutokea katika mazingira ya aina mbili. Kwanza, mazingira ya ugunduzi ambapo kitu kipya kilichogunduliwa hupewa jina. Pili, mazingira ya kuhamisha maarifa kutoka jamii moja hadi nyingine ambapo jamii inayopokea maarifa hulazimika kuunda istilahi kwa ajili ya kuyabeba maarifa hayo mapya. Katika mazingira haya lugha ya jamii yanakotoka maarifa huitwa lugha chanzi na ile ya jamii yanakopelekwa maarifa huitwa lugha lengwa. Uundaji wa istilahi katika mazingira ya aina ya kwanza huwa hauna maandalizi bali hutokea mara tu ugunduzi unapofanyika. Lakini uundaji wa istilahi katika mazingira ya pili huandaliwa kwa kuundiwa kanuni mahususi na wataalamu wa istilahi. Kanuni zinazoundwa husaidia katika ukusanyaji wa istilahi katika lugha chanzi, kuzifafanua kimaana, kuzitafutia visawe katika lugha lengwa na kusanifisha visawe hivyo. Uundaji wa istilahi za mradi wa KiLinux unaangukia katika mazingira ya aina ya pili.

 

ZINGATIA: Katika Mradi wa KiLinux:

     Uwanja wa maarifa ni Sayansi za kompyuta, eneo dogo la Programu endeshi za Linux.

     Lugha chanzi ni Kiingereza.

     Lugha lengwa ni Kiswahili.

 

 

2.0 Mazingatio katika maandalizi ya uundaji istilahi

 

Maandalizi ya uundaji wa istilahi hufanywa pale ambapo istilahi huundwa kwa ajili ya uhamishaji wa maarifa.

Maandalizi hayana kuzingatia mambo matatu:

        Uwanja wa maarifa.

        Waundaji wa istilahi.

        Lengo la uundaji wa istilahi.

 

2.1 Uwanja wa maarifa : Ubainishaji wa uwanja wa maarifa unatokana ukweli kwamba istilahi ni msamiati wa uwanja mahususi wa maarifa, kwa mfano, kompyuta, fizikia, kemia, hisabati, isimu nk. Uwanja wa maarifa unaweza kugawanywa zaidi katika maeneo madogomadogo. Kwa mfano uwanja wa kompyuta ukagawanywa katika: maunzi kompyuta, programu kompyuta; mawasiliano ya mtandao, vihariri vya matini nk. Ubainishaji wa uwanja wa maarifa hurahisi uainishaji wa maeneo na mifumo dhana katika uwanja husika. Kwa maneno mengi uwanja wa maarifa ndio msingi wa kubainisha seti ya istilahi zinazohusiana katika maarifa yanayohamishwa kutoka lugha chanzi.

 

2.2 Waundaji wa istilahi Ubainishaji wa waundaji istilahi ni muhimu kwa kuzingatia kwamba istilahi ni msamiati wa maarifa ya uwanja mahususi. Hivyo kazi ya uundaji istilahi huanza kwa kuutalii uwanja husika wa maarifa, kuugawa katika maeneo madogomadogo na kuunda mfumo wa dhana katika eneo husika kwa kuzingatia mahusiano kidhana. Kazi hiyo huhitaji ushirikiano wa karibu sana baina ya wataalamu wa maarifa husika na wale wa lugha. (Kwa upande wetu: wataalamu wa kompyuta na wa lugha ya Kiswahili). Kazi ya wataalamu wa maarifa husika ni kubainisha istilahi katika lugha chanzi kwa kuzingatia mfumo wa dhana na kufafanua dhana zinazobebwa na istilahi hizo. Ni muhimu kusisitiza hapa kwamba wataalamu wa maarifa hawana budi pia kuwa weledi wa lugha chanzi na lugha lengwa. Uweledi wao wa lugha chanzi utawasaidia katika kutoa fafanuzi zinazoeleweka kwa lugha hiyo na pia kuelewa tofauti za kikategoria za istilahi mbalimbali. Kwa upande wa lugha lengwa, weledi wao utasaidia katika kutathmini ubora wa visawe vya istilahi katika lugha lengwa. Kazi ya wataalamu wa lugha ni kutafuta visawe vya istilahi kwa kuzingatia ufafanuzi na uhusiano ya dhana kama ulivyobainishwa na wataalamu wa maarifa.

 

2.3 Lengo la uundaji istilahi

Uundaji wa istilahi unaweza kufanywa kwa ajili ya kukamilisha lengo mahususi, (mfano, tafsiri ya programu za Linux), au kwa ajili ya lengo pana kama vile kujenga hifadhi data ya istilahi za lugha lengwa. Pale ambapo uundaji wa istilahi ni kwa ajili ya kukamilisha lengo mahususi, kazi muhimu huwa ni kubainisha istilahi zote muhimu kwa kazi husika, kufafanua dhana za istilahi zilizokusanywa kwa kuzingatia uhusiano wa kidhana na kutafuta visawe vya istilahi zilizokusanywa kwa kuzingatia maana zilizofafanuliwa. Kwa kawaida kazi ya aina hii huwa imepangiwa muda maalum wa kuikamilisha. Uundaji wa istilahi kwa ajili ya hifadhi data ya lugha huwa hauna muda maalumu bali ni kazi ya kuendelea kwa muda mrefu.

 

ZINGATIA: Katika mradi wa KiLinux:

     Uwanja wa maarifa ni Sayansi za Kompyta katika eneo dogo la Programu Endeshi za Linux

     Waundaji istilahi ni timu ya wataalamu wa Sayansi za Kompyuta na timu ya wataalamu wa Isimu na Lugha ya Kiswahili

     Lengo la mradi ni kukamilisha kazi ya Uswahilishaji wa Programu za Linux kwa muda maalum.

 

 

3.0 Maana katika Lugha

 

Maneno ya lugha yanaweza kuhusishwa na maana za aina mbili: maana ya jumla na maana maalumu.

 

3.1 Maana ya jumla . Hii ni maana ya maneno katika mawasiliano ya kawaida ambapo wazungumzaji huelewa maana za maneno kama walivyoipata kutokana na uzoefu wao wa aina mbalimbali kama vile:

 

      kuona (mwonekano wa kitu) kompyuta ni mashine yenye kioo cha kuandikia

      kuonja (ladha ya kitu) sukari ni kitu kitamu

      kusimuliwa (kama alivyosikia) zimwi ni jitu kubwa lenye jicho na mguu mmoja

      kutumia (kazi ya kitu kompyuta ni mashine ya kuandikia na kusomea barua pepe

 

Jambo la kuzingatia hapa ni kwamba aghalabu watumiaji wa kawaida wa lugha hutumia maneno ya kitaalamu kwa kuyapa maana zisizo za kitaalamu.

 

3.2 Maana maalumu

Utaalamu ni maarifa na maarifa hubainishwa kwa kutumia lugha. Maneno yanayotumiwa na wataalamu wa uwanja mahususi kuelezea maarifa huitwa istilahi. Maana ya istilahi ni maalumu kwa sababu hufahamika tu kwa wataalamu wa maarifa husika. Kwa mfano, maana za istilahi za kompyuta, hufahamika tu kwa wataalamu wa kompyuta. Maana maalumu inayobebwa na istilahi huitwa dhana na ubainishaji wa sifa pambanuzi za dhana (ufafanuzi wa maana ya istilahi) huhitaji wataalamu wa maarifa husika.

Katika mfumo wa maarifa, mara nyingi istilahi huwa katika mahusiano kingazi ambapo istilahi zenye dhana pana hukaa juu ya zile zenye dhana mahususi. Istilahi za dhana mahususi hutokana na istilahi za dhana pana. Kadri istilahi inavyokuwa chini katika ngazi ya mahusiano ndivyo inavyokuwa na dhana mahususi zaidi. Istilahi ambayo dhana yake ni pana katika kiwango cha upeo wa juu kabisa hukaa juu kabisa katika ngazi ya mahusiano. Kwa kawaida istilahi ya namna hiyo huwa ya neno moja tu. Istilahi ya ngazi ya pili huwa na maneno mawili, ya ngazi ya tatu huwa na maneno matatu na ya ngazi ya nne huwa na maneno manne. Idadi kubwa ya istilahi iko katika ngazi ya pili.

 

Tazama mfano wa mahusiano kingazi:

 

1. kompyuta

 

kompyuta ndogo kompyuta kubwa kompyuta ya fremu

 

 

kompyuta ndogo ya IBM

kompyuta ndogo ya makintoshi

 

 

 

2. programu

 

programu za mikrosofti programu huria programu za makintoshi

 

3. mfumo

 

mfumo wa kompyuta

 

mfumo wa kompyuta ndogo

 

Tunachosisitiza hapa ni kwamba istilahi za uwanja mahususi wa maarifa huwa katika mfumo fulani wa mahusiano. Katika mahusiano hayo maana ya istilahi mahususi (zenye zaidi ya neno moja) inaweza kutazamwa katika sehemu mbili:

 

v     maana ambayo inahusisha istilahi na istilahi nyingine (maana ya istilahi pana ndani ya istilahi mahususi)

v     maana ambayo inabainisha upekee wa istilahi

Taz. swichi

 

swichi tafuti

 

swichi tafuti bendi

 

Neno swichi linapatikana katika istilahi zote hapo juu. Neno tafuti liko katika istilahi ya ngazi ya pili na ya tatu. Hili ndilo neno linalotofautisha istilahi hizi na ile ya juu kabisa. Istilahi ya ngazi ya tatu ina neno bendi ambalo ndilo linaloitofautisha na ile ya ngazi ya pili.

 

ZINGATIA: Aina mbili za maana:

     maana ya jumla

     maana maalum/kitaalamu (dhana)

Maneno yanayobeba maana maalumu huitwa istilahi

Maana mbili za istilahi

      maana pana

      maana mahususi

Uhusiano msonge wa istilahi:

      Istilahi zenye maana pana hukaa juu ya zile zenye maana mahususi

      Istilahi zenye maana pana huwa na maneno machache kuliko istilahi zenye maana mahususi.

 

4.0 Ufafanuzi wa maana katika istilahi

 

Ufafanuzi wa maana ya istilahi katika lugha chanzi ni hatua moja muhimu katika uundaji wa istilahi. Maana ya istilahi hufafanuliwa kwa kuzingatia:

 

4.1  Eneo la istilahi katika uwanja wa maarifa:

Ufafanuzi wa dhana za istilahi hufanyika baada ya kukusanya istilahi katika lugha chanzi. Ukusanyaji wa istilahi hufanywa baada ya kubainisha eneo mahususi la uwanja wa maarifa. Ufuatao ni mfano wa uwanja wa maarifa uliogawanya katika maeneo madogo.

Uwanja wa sayansi ya kompyuta

 

 

eneo la maunzi kompyuta eneo la programu

 

eneo la programu za Linux

 

Uwanja wa umeme

 

eneo la nishati eneo la maunzi

 

transfoma

 

 

Baada kubainisha eneo mahususi, kazi ya ukusanyaji hufanywa na wataalamu wa eneo husika. Baada ya kukusanya istilahi zote wataalamu hufafanua dhana ya kila istilahi. Ufafanuzi hufanywa katika lugha chanzi. Hivyo wataalamu wanaofafanua istilahi hawana budi kuielewa vizuri lugha chanzi ili waweze kufafanua dhana za istilahi vizuri kwa kuzingatia usahihi wa dhana na kategoria ya istilahi

 

4.1.1        Dhana sahihi ya istilahi

 

Ni dhahiri kwamba kama mtaalamu haijui vilivyo lugha chanzi, itamwia vigumu kutambua maana halishi ya istilahi katika lugha hiyo. Kutotambua maana halisi ya istilahi katika lugha chanzi kutasababisha kutoa tafsiri isiyo sahihi. Wakati mwingine maana za kawaida katika lugha chanzi hupewa hadhi ya dhana katika uwanja mahususi. Kwa mfano katika Kiingereza, mouse limepewa dhana mahususi katika kompyuta tofauti na maana yake ya kawaida ambayo kwa Kiswahili ni puku ( panya pori). Hivyo kuelewa maana ya msingi katika lugha chanzi husaidia katika kujenga uhusiano wa maana hiyo na ile ya kiistilahi.

 

4.1.2        Kategoria ya istilahi

Kutambua kategoria ya istilahi ni kubaini kama istilahi ni nomino au kitenzi au kivumishi. Kwa kawaida istilahi nyingi ni za kategoria ya nomino au kwa lugha ya kawaida ni majina. Hata hivyo kuna istilahi ambazo ni za kategoria ya kitenzi na hata kivumishi. Umbo moja la istilahi kama drive linaweza kuanishwa katika kategoria mbili tofauti, za ama nomino au kitenzi. Kutambua kategoria halisi ya istilahi ni muhimu kwa vile maana ya istilahi katika kategoria mbili hutofautiana. Kwa mfano,

 

drive (nomino) kiendeshi

drive (kitenzi) endesha

 

Endapo mtaalamu wa maarifa husika atashindwa kubainisha kategoria halisi ya istilahi kuna hatari ya kutoa maana isio halisi.

 

 

4.2. Uhusiano wa istilahi kingazi

 

Ufafanuzi wa maana za istilahi katika lugha chanzi hauna budi kuzingatia uhusiano wa kingazi wa istilahi. Kama ambavyo imekwishaonyeshwa hapo awali, istilahi za kikoa fulani cha maana huwa na uhusiano wa kingazi ambapo istilahi ya ngazi ya juu huwa na maana pana zaidi kuliko ile ya ngazi ya chini. Kwa hiyo maana ya istilahi ya ngazi ya juu huwa pia katika istilahi ya ngazi ya chini. Hata hivyo istilahi ya ngazi ya chini pamoja na kuwa na maana ya istilahi ya ngazi ya juu huwa pia na maana ya ziada inayoipambanua na ili ya ngazi ya juu. Kwa maneno mengine maana pana ya istilahi huonyesha uhusiano wa istilahi na istilahi nyingine katika uhusiano wa kingazi na maana pambanuzi huonyesha upekee wa istilahi ya ngazi ya chini. Kutozingatiwa kwa uhusiano wa maana kingazi katika ufafanuzi wa maana za istilahi katika lugha chanzi husababisha kutokubaliana kimaana kwa istilahi zinazohusiana.

 

4.3. Mbinu za ufafanuzi wa maana ya istilahi.

 

Zifuatazo ni baadhi ya mbinu zinazotumika katika kufafanua maana ya istilahi katika lugha chanzi:

 

4.3.1 Kufafanua kwa uchanganuzi

 

Mfano: lugha programu = lugha inayotumika kuandikia programu za kompyuta

 

Aina hii ya ufafanuzi hutoa maana kwa kuchanganua sifa za aina fulani zinazopambanua istilahi kwa njia ya maelezo. Ufafanuzi unaweza kuwa ni wa kikazi, kiumbo, kimchakato

 

4.3.2 Kufafanua kwa sinonimia

Kwa mfano: kompyuta = tarakilishi au ngamizi

televisheni = runinga

 

 

Katika njia hii ya ufafanuzi maana hautolewi. Kwa vyovyote vile njia hii haimwezeshi mtu asiye mtaalamu wa maarifa husika kujua maana ya istilahi.

 

4.3.3. Kufafanua kwa kwa kutumia maneno mengine ( paraphrasing)

 

Kwa mfano: bofya = kubonyeza puku mara moja

: bofyabofya = kubonyeza puku mara mbili bila kusita.

 

Njia hii pia haifafanui maana katika hali itakayomsaidia mtu asiye mtaalamu.

 

 

4.3.4. Kufafanua kwa kutoa sifa nyingi pamoja (synthesis)

Njia hii hutoa maana kwa kutaja kwa pamoja sifa mbalimbali kama vile za umbo, kazi, rangi nk.

Hii ni njia nzuri kwa vile hujumuisha sifa nyingi kwa pamoja na kutoa picha halisi zaidi kwa mtu asiye mtaalamu wa uwanja husika.

 

4.3.5. Kufafanua kwa kuorodhesha mifano (listing examples)

Kwa mfano : kompyuta = kompyuta ndogo, kompyuta kubwa, kompyuta za fremu

Njia hii sio nzuri kwani hafafanui maana bali hutoa mifano tu

 

4.3.6. Kufafanua kwa kutumia vielelezo (demonstration)

Mfano wa vielelezo ni kama vile michoro, picha nk

Njia hii ni nzuri kama itatumika pamoja na maelezo.

 

ZINGATIA:

 

Ufafanuzi sahihi wa maana za istilahi katika lugha chanzi ndio msingi wa uundaji wa visawe vya istilahi katika lugha lengwa.

Kwa vipi?

      hutoa picha halisi ya istilahi katika mfumo wa maarifa

      husaidia katika ubainishaji wa istilahi zote zinazohusiana

      huwapatia wataalamu wa lugha maana ya kitaalamu

      husaidia wataalamu wa maarifa kufanyia tathmini visawe vilivyopendekezwa.

 

5.0 Maana katika uundaji wa visawe

 

Kazi ya kuunda visawe vya istilahi katika lugha lengwa hufanywa na wataalamu wa lugha lengwa. Hata hivyo wataalamu hao wanapaswa pia kuifahamu vizuri lugha chanzi ili waweze kuelewa maana za istilahi katika lugha chanzi kama zilivyofafanuliwa na wataalamu wa maarifa husika. Wataalamu wa lugha lengwa wanapoelewa maana ya istilahi katika lugha chanzi hurejea katika utaalamu wao wa lugha lengwa na kutafuta visawe vya istilahi zilizofafanuliwa. Mbinu mbalimbali zinazotumika kutafuta visawe ni kama hizi zifuatazo:

 

5.1 Kutohoa

Kutohoa ni kuchukua umbo la istilahi katika lugha chanzi na kulipa umbo la lugha lengwa:

Kwa mfano:

Komputer kompyuta

Program programu

 

Screen skrini

 

Katika mifano hiyo hapo juu, istilahi za Kiingereza zimetoholewa kwa kupewa maumbo ya maneno ya Kiswahili

 

 

5.2 Kubuni

Mbinu hii ya kubuni inaweza kufanywa kidhahania au kwa kutumia vigezo mahususi.

 

5.2.1 Kidhahania

Mbinu ya kubuni visawe kidhahania hutetewa kwa hoja kuwa hakuna uhusiano wa moja kwa moja baina ya istilahi na dhana inayobebwa. Hivyo neno lolote linaweza kuundwa na kupewa hadhi ya istilahi ya dhana fulani. Njia mojawapo ya kuunda maneno kidhahania ni kutumia fomula za kikompyuta ambapo maneno mengi yanaweza kuzalishwa na kupachikwa dhana mahususi katika uwanja fulani wa maarifa.

 

5.2.2 Kivigezo

Kubuni visawe huweza kufanywa kwa kutumia vigezo mahususi kama vile kazi, umbo, au mwonekano wa kitu. Kwa mfano kwa kutumia kigezo cha kikazi, kisawe cha calculator kimebuniwa kuwa ni kikokotozi, (kitu kinachofanya kazi ya kukokotoa); kisawe cha data saver kimekuwa kihifadhi data, (kitu kinachohifadhi data). Vipo pia visawe vingine kama vile tarakilishi (computer) na runinga (television) ambavyo vimeundwa kwa kutumia vigezo mahususi.

 

5.3 Kupanua maana

Njia hii huchukua neno lenye maana ya jumla na kuliongezea maana ya kiistilahi katika mazingira ya kitaalamu. Kwa mfano, neno puku ambalo katika maana ya jumla ni panya pori, katika mazingira ya utaalamu wa kompyuta limepewa maana ya kiistilahi kama kisawe cha mouse. Mfano mwingine ni wa neno kifaru, ambalo maana yake ya jumla ni mnyama lakini katika mazingira ya utaalamu wa kijeshi ni kisawe cha tank.

 

 

Jambo la msingi hapa ni kuwa waundaji wa visawe vya istilahi hupaswa kufahamu vyema maana ya istilahi katika lugha chanzi na pia kuwa na utaalamu wa kutosha wa mofolojia, leksika na sintaksia ya lugha husika. Visawe vinavyoundwa na wataalamu wa lugha havina budi kuhakikiwa na wataalamu wa maarifa husika na kuthibitishwa kuwa vinabeba dhana zilizokusudiwa kikamilifu. Hivyo kwa upande mwingine wataalamu wa uwanja wa maarifa wanapaswa pia wawe mahiri katika lugha lengwa ili waweze kutathmini vizuri visawe vilivyoundwa.

 

ZINGATIA

Katika uundaji wa visawe vya istilahi za programu huria za Linux, wataalamu wa Kiswahili hutumia mbinu mbalimbali kama vile

      Kutohoa na

      Kubuni

Vilevile wataalamu wa kompyuta wanapaswa kupitia visawe vilivyopendekezwa ili kuthibitisha kwamba vinabeba dhana zilizokusudiwa kikamilifu. Kwa hali hiyo wataalam hao wanapaswa kuifahamu vizuri lugha ya Kiswahili (lugha lengwa) kama vile wanavyostahili kuifahamu vizuri lugha ya Kiingereza (lugha chanzi).

 

 

6.0  Mwisho

 

Mada hii ya mafunzo imewasilishwa kwa lengo la kuwasaidia watafiti wasaidizi katika kazi ya kuunda istilahi za mradi wa Kuswahilisha programu huria za Linux. Uwasilishaji umezingatia kipengele cha maana katika kazi ya utafutaji wa istilahi katika lugha chanzi na uundaji wa visawe vya istilahi hizo katika lugha lengwa. Mambo yaliyotiliwa mkazo hapa ni kuzingatia kuwa kazi ya uundaji istilahi hufanywa kwa lengo la kuhamisha maarifa kutoka jamii moja kwenda nyingine. Katika kufanya kazi hiyo, wataalamu wa maarifa hubainisha istilahi husika katika lugha chanzi na kufafanua maana zake kwa kuzingatia uhusiano wa maana kingazi. Baada ya ufafanuzi, huwapelekea wataalamu wa lugha lengwa ili waweze kuunda visawe vya istilahi husika. Kazi hii hufanywa kwa kuzingatia kwa makini ufafanuzi wa maana kama ulivyotolewa na wataalamu wa maarifa husika.

 

 


MAREJEO

 

(-) 1997. ISO CD 704 Terminology work Principles and Methods

 

Sager, J. C. 1990. Practical Course in Terminology Processing: Amsterdam & Philadelphia: Benjamins Publishing Company.