July 13, 2005 11:33 AM

Jambo OpenOffice katika Maonesho ya 29 Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam

Katika Maonesho ya 29 Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam Timu ya Kilinux ilipata
fursa ya kuonesha toleo la kwanza la Kiswahili la OpenOffice.org 1.1.3 liitwalo Jambo.

Watu wengi kutoka nje na ndani ya Tanzania wanashangaa waonapo program hii na kuthamini
juhudi za timu ya Kilinux katika uswahilishaji wa Programu Huria. Wengi wao waliichukua
programu na wengine walichukua anuani ya tovuti ili waende kupakua Jambo OpenOffice moja
kwa moja kutoka kwenye mtandao.

Watu walivutiwa sana kutumia programu hii mpya kwasababu si kwamba itarahisisha kazi
zao tu bali pia itapunguza muda wa kuzifanya kazi hizo. Kazi zitafanyika kwa ufanisi
zaidi hususani shughuli za kuandaa maandiko, mawasilisho, ripoti, michoro n.k. katika
lugha ya Kiswahili ambayo ni muhimu sana Afrika ya Mashariki na Kati na sehemu
nyingine ulimwenguni. Watu walielewa pia faida za kutumia Programu Huria kulinganisha
na Programu funge. Wengi wao walikua hawazifahamu Programu Huria. Waliahidi kuja
idara ya Sayansi ya Kompyuta kujionea nini kinaendelea na kuchukua programu hii.

Watu wengine kutoka Afrika ya Mashariki na Kati wameshachukua programu hii,
watu kutoka Ulaya mathalani Ujerumani, Ubeligiji n.k. na Marekani walisema wanatumia
sasa hivi Jambo OpenOffice nchini mwao. Timu ya Kilinux inawashukuru kwa kukubali
programu za Kiswahili na inaahidi kuendelea na mchakato wa uswahilishaji mpaka mfumo
kamili wa uendeshaji kwa Kiswahili utakapotokea.


Imetumwa na James Chambua | Kategoria: HABARI, OPENOFFICE